Swali linaloonekana kuwasumbua Watanzania kuna nini ikulu? || Panga pangua | Maandalizi ya uchaguzi

Kuna nini Ikulu? Ndilo swali linaloonekana kuwasumbua Watanzania wengi kwa sasa, baada ya Rais Samia Suluhu Hassan kufanya mabadiliko mengi mfululizo ya wasaidizi wake katika kipindi kifupi, kati ya Mei na Juni mwaka huu.
Katika kipindi hicho, mkuu huyo wa nchi amefanya mabadiliko ya wasaidizi wake 10, wanane kwa Juni pekee na wawili Mei, mwaka huu.
Mabadiliko hayo yanahusisha kuwaondoa baadhi ya wasaidizi wake katika Ofisi ya Rais Ikulu na kuwateua katika mamlaka, idara na taasisi nyingine mbalimbali za Serikali.
Wakati wengi wakihoji kunani nyuma ya mabadiliko hayo, wanazuoni wa siasa na uongozi, wanahusisha mabadiliko yanayofanywa ama na harakati za kuelekea uchaguzi, kuziba ombwe la wasiowajibika au kuongeza ufanisi.
Wanataaluma wengine wamekwenda mbali zaidi na kuyafananisha mabadiliko hayo na kile walichokiita usafishaji wa nyumba iliyochafuka kitambo.
Ingawa ni mamlaka ya Rais kuanzisha na kufuta nafasi za madaraka mbalimbali katika utumishi, kwa mujibu wa Ibara ya 36(1) ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, bado uamuzi wake unaibua mijadala.
Mijadala zaidi katika mitandao ya kijamii iliibuka katika mabadiliko aliyofanya Juni 6, 2024 alipomhamisha Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais Ikulu, Zuhura Yunus kwenda kuwa Naibu Katibu Mkuu Ofisi ya Waziri Mkuu, Kazi, Vijana na Wenye Ulemavu.
Panga pangua Ikulu ilianza siku chache tu baada ya Rais Samia kuapishwa kushika wadhifa huo, Machi 19, 2021 kuchukua nafasi ya Rais John Magufuli aliyefariki dunia Machi 17 mwaka huo.
Baada ya kuapishwa alimwondoa aliyekuwa Katibu Mkuu Kiongozi, Dk Bashiru Ally na kumteua kuwa mbunge huku nafasi yake ikichukuliwa na Balozi Hussein Kattanga Machi 31, 2021.
Aprili 4, 2021 alimuondoa Gerson Msigwa katika wadhifa wa Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais, Ikulu, baada ya kuhudumu kwa miaka sita tangu Agosti mwaka 2016 wakati wa utawala wa Magufuli na kumteua kuwa Mkurugenzi wa Idara ya Habari Maelezo na Msemaji Mkuu wa Serikali.
Nafasi aliyokuwa nayo Msigwa ndani ya ofisi hiyo nyeti ilirithiwa na Jaffar Haniu aliyeteuliwa Juni mwaka 2021 lakini naye hakudumu, Februari ya mwaka uliofuata aliondolewa na kwenda kuwa Mkuu wa Wilaya Rungwe, akimpisha Zuhura Yunus.
Katika panga pangua hiyo, Moses Kusiluka aliteuliwa kuwa Katibu Mkuu Ikulu na Januari 2023 Diwani Athumani aliteuliwa kumrithi. Diwani alidumu kwa siku mbili tu, baadaye nafasi hiyo ilirithiwa na Mululi Mahendeka anayeongoza hadi sasa.
Ingawa haionekani kama ni ofisi ya moja kwa moja Ikulu, lakini Agosti 28, 2023 Rais alifanya mabadiliko ya mkurugenzi mkuu wa usalama wa Taifa na kumteua Ali Idi Siwa akichukua nafasi ya Said Hussein Massoro aliyehudumu kwa miezi minane.
Tangu mabadiliko hayo, umma haukushuhudia mabadiliko ya mara kwa mara kwa wasaidizi wa Rais hadi Mei na Juni 2024, miezi inayoonekana kuvunja rekodi ya hamishahamisha hadi baadhi ya watu kuanza kuhoji kuna nini Ikulu?
Januari 2024, Rais Samia alimhamisha ofisa mwandamizi Ofisi ya Rais Ikulu, Doris Kalasa na kumteua kuwa Katibu Tawala (RAS) mkoa wa Iringa.
Mei 29,2024, Rais akamhamisha Dk Linda Ezekiel aliyekuwa Kaimu ofisa mtendaji mkuu wa President’s Delivery Bureau (PDB) kwenda kuwa naibu katibu mkuu mtendaji, Tume ya Mipango nchini, anayeshughulikia ubunifu wa biashara.
Juni 6, Rais akamhamisha Felister Mdemu aliyekuwa msaidizi wa Rais (Maendeleo ya Jamii) kwenda kuwa naibu katibu mkuu Maendeleo ya Jamii na Zuhura Yuhus kutoka mkurugenzi wa mawasiliano Ikulu kwenda kuwa naibu katibu mkuu.
Pia tarehe hiyohiyo, akamuondoa Petro Magoti aliyekuwa msaidizi wa Rais (siasa) kwenda kuwa mkuu wa Wilaya Kisarawe na akamhamisha pia Nehemia Mandia aliyekuwa Msaidizi wa Rais (sheria) na kumteua kuwa jaji wa Mahakama Kuu.
Halikadhalika, Juni 11, 2024 akamwondoa msaidizi mwingine Elias Mwandobo kwenda kuwa mkuu wa Wilaya ya Momba.
Juni 15,2024, akamhamisha Balozi John Simbachawene aliyekuwa ofisa mwandamizi Ofisi ya Rais, Ikulu kwenda kuwa naibu katibu mkuu wizara ya Viwanda na Biashara na pia Dk Habib Kambanga mwenye wadhifa kama huo kuwa balozi.
Pia akamhamisha Ofisa Mwandamizi wa Ofisi ya Rais Ikulu, Mkoba Mabula, kwenda kuwa Naibu Katibu mkuu katika wizara ya Maliasili na Utalii, wizara ambayo huwa mawaziri wake pia huwa hawadumu muda mrefu.

Пікірлер: 5

  • @user-jn3nf7uw1w
    @user-jn3nf7uw1w21 күн бұрын

    Kazi iendeleeeeeeee++++

  • @froma3732
    @froma373221 күн бұрын

    Kama amechaguwa kutokana Ushauri wanohusika yeye anapitisha lkn ikiwa hakupendezwa na Kazi yako inabidi uwende kama Hilo linakusumbuwa itakupa tabu sana

  • @gasperswai6963
    @gasperswai696321 күн бұрын

    Kwani kuna shida gani kama wasaidizi wake kama wana uwezo wa kufanya makubwa zaidi ya hapo walipo kuna shida gani, kwenye management kuna issue ya capacity building! Hakuna aja ya kuwa na team amblyopia wanaweza kucheza zaidi kwenye maeneo unajua kuna gap! Mhe rais bado hupo vzr

  • @MageAwe-hl5zb
    @MageAwe-hl5zb21 күн бұрын

    Huko ni kujidanganya hakuna mwanadamu aliyekamilika

  • @NassoroSipemba
    @NassoroSipemba21 күн бұрын

    Hilo swali lako halina kichwa wala miguu, kwani hakuna la ajabu hapo Rais anafanya hapendavyo kwani hilo limo ndani ya uwezo wake.

Келесі